Wakati
juhudi za kuisaka ndege iliyopotea ilipokuwa ikisafiri kutoka Malasyia
kuelekea Uchina zikiendelea, ndege moja ya Vietnam imeripoti kuwa imeona
kitu kinachofanana na mlango wa ndege kwenye ufuo wa bahari ya Kusini
mwa Uchina kwenye mwambao wa taifa hilo.
Hata
hivyo hakuna thibitisho kuwa mlango huo ni wa ndege iliyopotea ya
Malaysia, iliyokuwa na abiria mia mbili na thelathini na tisa.
Uchunguzi
kuhusiana na kilichosababisha kupotea kwa ndege hiyo mapema siku ya
Jumamosi, inawalenga abiria wawili wanaodaiwa kuwemo ndani ya ndege
hiyo, waliotumia paspoti iliyoibiwa.
Stakabadhi hizo mbili za kusafiria kutoka Italia na nyingine Australia inaaminika kuibwa nchini Thailand.
Idara ya polisi ya Kimataifa, Interpol, inasema kuwa ni mapema mno kuhusisha pasi zilizoibwa na kutoweka kwa ndege hiyo.
Na huku
kushughuli za kuisaka ndege hiyo zikiendelea, Msemaji wa shirika la
ndege la Malysia amewaambia jamaa ya watu waliokuwemo katika ndege hiyo,
kujiandaa kwa taarifa mbaya.
Wakuu wa
Malysia wanasema jumla ya meli 30 na ndege 44 kutoka mataifa tisa
tofauti duniani, yamejiunga katika shughuli za kuitafuta ndege hiyo.
Kamanda
William Marks wa kikosi cha saba cha jeshi la wanamaji la Marekani,
ametuma ndege aina ya USS Pinckney kusaidia katika usakaji huo.
''Jambo
la kwanza kufanywa ni kukadiria mahala na kwa sasa tunalenga mawasiliano
ya mwisho kutoka kwa ndege hiyo kabla ya kutoweka na mawasiliano ya
rada. Kutoka hapo tunahesabu mwendo kasi ya upepo na mawimbi. Kutoka
hapo tunagawanya na eneo na tunatafuta kutumia kila kifaa tuliyonayo- na
hiyo siyo tu kutumia vifaa kutoka Marekani lakini pia kutumia meli na
anga kutoka mataifa mengine ya dunia." Alisema kamanda huyo.
Ameonya kuwa shughuli hiyo ya kutafuta ndege hiyo inakumbwa na changamoto nyingi.Chanzo BBC Swahili.
0 comments:
Post a Comment